Pages

Thursday, May 10, 2012

TANESCO yaisamehe Zanzibar deni la bilioni 50/-

Default TANESCO yaisamehe Zanzibar deni la bilioni 50/-

WAKATI Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) likipandisha bei ya umeme kwa matumizi ya kawaida kwa wananchi kwa asilimia 40, imethibitika kwamba limefutiwa deni lake la muda mrefu kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), linalofikia zaidi ya Sh bilioni 50.

Meneja Mkuu wa Zeco Hassan Ali Mbarouk alithibitisha kufutwa kwa deni hilo alipokutana na waandishi wa habari jana na kusema hali hiyo inatokana na ushirikiano mzuri kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mbarouk alisema deni hilo lilifutwa baada ya uongozi wa shirika hilo kuwasilisha malalamiko yake ya muda mrefu na baadaye kukutana na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, na kupitia malalamiko yote na kuonekana kwamba deni hilo halina uhalali wa kuwapo.

Uongozi wa Zeco ulikuwa ukipinga ongezeko la bei ya umeme ambayo iliongezwa mwaka 2008.

“Tunamshukuru sana Waziri aliyekuwepo wakati ule (Ngeleja), alikutanisha pande mbili, Tanesco na Zeco na kusikiliza malalamiko na alikubaliana nasi na kutaka kufutwa kwa deni hilo kabla ya kuingizwa katika kero za Muungano,” alisema Mbarouk.

Alifafanua kuwa tatizo hilo limepatiwa ufumbuzi wa kudumu na sasa Zeco imekuwa ikilipa umeme inaonunua Tanzania Bara kwa awamu, lakini hawana deni linalotokana na malimbikizo au kubambikiziwa.

“Tunalo deni la kawaida tu kutoka kwa Tanesco la kununua umeme…hatuna deni linalotokana na utata wa kubambikiziwa,” alieleza Meneja huyo. Mapema, Shirika la Umeme Zanzibar lilieleza kwamba lipo katika hatua ya kutekeleza miradi miwili ya kuongeza vituo vya kusambaza umeme Unguja na kufadhiliwa na Serikali ya Japan.

Mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Japan ni kwa ajili ya kujenga vituo vitatu vya kusambaza umeme kikiwamo cha Mpendae ambacho kitakuwa kikisambaza umeme katika ukanda wa Uwanja wa Ndege na Chukwani ambayo imekuwa ikikabiliwa na tatizo la kuzidiwa nguvu.

Meneja huyo wa Zeco alisema bado wanaendelea na mikakati ya kutafuta wawekezaji katika miradi ya umeme mbadala kwa lengo la kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana.

Source: Habari leo

My Take: Inasamehe madeni wakati yenyewe kila siku inalia njaa na kukopa mabilioni katika mabenki

No comments:

Post a Comment