TANESCO yaisamehe Zanzibar deni la bilioni 50/-
WAKATI
Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) likipandisha bei ya umeme kwa matumizi
ya kawaida kwa wananchi kwa asilimia 40, imethibitika kwamba limefutiwa
deni lake la muda mrefu kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),
linalofikia zaidi ya Sh bilioni 50.
Meneja
Mkuu wa Zeco Hassan Ali Mbarouk alithibitisha kufutwa kwa deni hilo
alipokutana na waandishi wa habari jana na kusema hali hiyo inatokana na
ushirikiano mzuri kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Mbarouk
alisema deni hilo lilifutwa baada ya uongozi wa shirika hilo
kuwasilisha malalamiko yake ya muda mrefu na baadaye kukutana na
aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, na kupitia
malalamiko yote na kuonekana kwamba deni hilo halina uhalali wa kuwapo.
Uongozi wa Zeco ulikuwa ukipinga ongezeko la bei ya umeme ambayo iliongezwa mwaka 2008.
“Tunamshukuru
sana Waziri aliyekuwepo wakati ule (Ngeleja), alikutanisha pande mbili,
Tanesco na Zeco na kusikiliza malalamiko na alikubaliana nasi na kutaka
kufutwa kwa deni hilo kabla ya kuingizwa katika kero za Muungano,”
alisema Mbarouk.
Alifafanua
kuwa tatizo hilo limepatiwa ufumbuzi wa kudumu na sasa Zeco imekuwa
ikilipa umeme inaonunua Tanzania Bara kwa awamu, lakini hawana deni
linalotokana na malimbikizo au kubambikiziwa.
“Tunalo
deni la kawaida tu kutoka kwa Tanesco la kununua umeme…hatuna deni
linalotokana na utata wa kubambikiziwa,” alieleza Meneja huyo. Mapema,
Shirika la Umeme Zanzibar lilieleza kwamba lipo katika hatua ya
kutekeleza miradi miwili ya kuongeza vituo vya kusambaza umeme Unguja na
kufadhiliwa na Serikali ya Japan.
Mradi
unaofadhiliwa na Serikali ya Japan ni kwa ajili ya kujenga vituo vitatu
vya kusambaza umeme kikiwamo cha Mpendae ambacho kitakuwa kikisambaza
umeme katika ukanda wa Uwanja wa Ndege na Chukwani ambayo imekuwa
ikikabiliwa na tatizo la kuzidiwa nguvu.
Meneja
huyo wa Zeco alisema bado wanaendelea na mikakati ya kutafuta
wawekezaji katika miradi ya umeme mbadala kwa lengo la kuhakikisha umeme
wa uhakika unapatikana.
Source: Habari leo
My Take: Inasamehe madeni wakati yenyewe kila siku inalia njaa na kukopa mabilioni katika mabenki
Source: Habari leo
My Take: Inasamehe madeni wakati yenyewe kila siku inalia njaa na kukopa mabilioni katika mabenki